Ukurasa wa nyumbani
 Uhamashishaji




Fasiri:

Bahasa Indonesia
বাংলা / Baṅla
Català
English
Español
Filipino/Tagalog
Français
Galego
Ελληνικά / Elliniká
हिन्दी / Hindī
Italiano
日本語 / Nihongo
Kiswahili
Polszczyzna
Português
Română
Русский
Српски / Srpski
Tiếng Việt
اردو / Urdu

                                        

Kurasa nyingine:

Visomo

Ramani ya tovuti

Maneno muhimu

Wasiliana nasi

Nyaraka za matumizi

Tovuti zinazohusiana

UFAFANUSI WA KIPINDI CHA UHAMASHISHAJI

na Phil Bartle, PhD

imetafsiriwa na Wamalwa Philip


Vifaa vya Mafunzo na Marejeleo

Vipengele vya kila hatua katika kipindi

Kwa ufupi:

Makala haya yanaangazia kila hatua katika kipindi cha uhamashishaji. Kila kipindi kinafafanuliwa kwa ufupi. Ni vyema makala haya yasomwe pamoja na Kipindi cha Uhamashishaji ukurasa mmoja wa kijitabu cha mafunzo. Kipindi hiki kimeelezwa kwa michoro hapa Michoro ya Kipindi cha Uimarishaji


Kipindi cha Uhamashishaji

Utangulizi:

Kipindi cha uhamashishaji mara nyingine huitwa "Kipindi cha Kukuza Ushirika wa Jamii," au "Kipindi cha Kitatua Shida," au "Kipindi cha Maendeleo ya Jamii," au "Kipindi cha Kusisimua Jamii." Hii ni misururu ya miradi (ambayo inatekelezwa na mhamashishaji mmoja au zaidi) ili kuongeza kiwango cha ushiriki wa jamii katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii hiyo.

Inaitwa "Kipindi" kwasababu hurudiwa rudiwa kila mara ikizingatiwa mafanikio, makosa na maarifa yaliyosomwa kutoka kwa miradi ya awali.

Kipindi:
  • Hii ni misururu ya miradi iliyopangwa kwa ustadi kutoka kiwango cha chini kuendelea mbele;
  • Huelekezwa na kusimamiwa na mhamashishaji au (wahamashishaji) ambaye ni halali, ameidhinishwa na kutambulika;
  • Hutumia njia ya kushirikiana na jamii kama mbinu ya kuimarisha jamii na wala si kama lengo la mwisho;
  • Inahitaji kuwa mhamashishaji (au wahamashishaji) wanaujuzi wa kutosha na wanaelewa na kuzingatia tabia nyeti za jamii;
  • Inaweza kuelekezwa na kusimamiwa na wizara au idara ya serikali katika wilaya au na sharika lisilo la kiserikali;
  • Asili yake si ya "kutoka chini mpaka juu", ya kijamii au "ya mashinani", lakini malengo yake ni kuimarisha jamii "kutoka chini hadi juu" au kutoka "mashinani"; na
  • Inakuza (inatia moyo, inatetea au kupigania, inafundisha ujuzi unaotakiwa, na inaunga mkono) kushiriki kwa jamii katika usimamizi na maamuzi yote yanayohusu au kuadhiri jamii kwa jumla.

Hatua kuu:
  • Kila hatua katika kipindi imeunganishwa kwa ustadi na hatua nyingine na kwa kipindi chote;
  • Zote ni muhimu (ukosefu wa moja wapo wa hatua itaadhiri kwa kiwango kikubwa matokeo yake);na
  • Zinahitajika kutekelezwa kwa mpangilio ufuatao, hata ingawa kunaweza kuwa na uwiiano na mfululizo.

Ni muhimu kuhakikisha kushiriki kwa watu wote wa jamii iliyolengwa (bila kuzingatia tabia yao ya kijamii au kimaumbile) ili kupata mafanikio mema katika kuondoa umaskini na kuimarisha jamii. Hapa katika mradi wa CDP "kushiriki," hasa inamaanisha kushiriki kwa jamii kikamilifu katika maswala yote ya usimamizi na maamuzi ya miradi ya jamii (wala sio kushiriki kwa mambo fulani machache tu).

Maamuzi muhimu ambayo lazima kufanywa na kusimamiwa ni pamoja na yafuatayo: kukadiria mambo (mahitaji na uwezo); kutambua shida za dharura (na kubuni malengo na nia kwa kuzingatia shida hizo); kupanga mikakati (yaani mipango na mbinu ya jamii): kutekeleza na kufuatilia miradi hiyo, na kukadiria matokeo yake.

Jamii kwa jumla inachukua jukumu ( (wala haistahili kuachia mtu wa nje).

Mchango wa rasilimali (kwa mfano michango ya pesa, kazi ya kijitolea na vifaa vingine), mazungumzo na mashauriano na mashirika ya nje ni muhimu, ijapokuwa tunaposema "kushiriki" (katika muktadha huu wa kushiriki kwa jamii) tuna maana zaidi na kamilifu kuliko tu "kuchanga" au "kushauriana."

Kuhamasisha na Kupokea Vibali:

Wahamashishaji wa jamii lazima wawe wanatambuliwa na viongozi wa serikali na kupokea vibali vyote vinavyohitajika kisheria ili waepuke kushikwa na polisi na maafisa wengine wa serikali kwa kudhaniwa kuwa ni wachochezi wa kisiasa.

Pia, inafaa kueleweka kuwa ni viongozi wengi wa serikali ndio hupendelea mbinu ya "kupeana" na huogopa sana mbinu ya "kuwezesha", kwasababu wafanyi kazi wa serikali, maafisa, wanasiasa, viongozi wa jadi na wanaochipuka na hata wataalamu wa kiufundi huona manufaa ya haraka ya kujipatia sifa na ushawishi, kura, kupanda cheo na kujiendeleza katika taaluma zao kwa kutumia mbinu ya kupeana. Kwa hivyo, uhamashishaji ni muhimu sio tu kama njia ya kufanya vitu kirasmi, la; lazima ipangwe na kutekelezwa vizuri. Hivyo basi, kukabiliana na uvumi na fikira au dhana za uongo lazima iwe miongoni mwa mikakati ya uhamashishaji.

Kukuza Ufahamu:

Kabla ya kuisaidia jamii kushiriki kwa mradi fulani (na hivyo basi kujifunza na kupata nguvu na uwezo zaidi) mhamashishaji lazima aiambie jamii hiyo ukweli wa mambo ya kimsingi ambayo watahitajika kufanya.

Katika hatua hii, ni muhimu kujizuia kuleta matumaini ya uongo, na kukabiliana kwa dhati na fikira au dhana pamoja na uvumi kuhusu aina ya msaada ambao utaletwa.

Ufahamisho huo lazima uwe na vipengele kama vile:
  • Ikiwa wana jamii watazembea na kutegemea msaada wa serikali au msaada kutoka nje, basi daima watabakia na mzigo wa umaskini na unyonge;
  • Hakuna jamii ambayo ni maskini kabisa; ikiwa kuna binadamu hai, basi jamii hiyo ina rasilimali na uwezo, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kufanya kazi, ubunifu, uhai, matumaini, mbinu za kuishi na utamaduni;
  • # Ni rahisi watu kujiunga na kusaidia mradi ikiwa wewe kama mhamashishaji tayari unajisaidia mwenyewe; na
  • Mhamashishaji (na shirika au idara yake) hawaleti rasilimali (kama vile pesa,vifaa vya kuezeka nyumba, pombo na kadhalika), mbali wanatakiwa kuelekeza na kusaidia katika usimamizi, mafunzo na ushauri.

Kuleta Umoja:

Hakuna jamii ambayo huwa umoja kamili; lazima kuwepo na migawanyiko na vikundi katika kila jamii.. Ukubwa wa migawanyiko hiyo hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine.. Ikiwa kuna tofauti kubwa katika jamii, basi huwa vigumu kufikia makubaliano kuhusu ni miradi ipi ipewe kupao mbele, na malengo ya muhimu.

Kuleta umoja lazima itangulie uhamashishaji wa jamii, na huendelea katika kipindi chote. Tazama Kuleta Umoja.

Mafunzo ya Mhamashishaji:

Wahamashishaji wachache walioko hawawezi kuifikia kila jamii ambayo inahitaji uhamashishaji ili kukuza uwezo wake na kuifanya iwe ya kujitegemea. Katika mradi wa Uganda CMP, kulikuweko na wahamashishaji kumi katika kila parokia. Hawa walikua wafanyikazi wakujitolea bila malipo na ambao awali walikuwa miongoni mwa kikundi cha Resistance Movement (yaani vuguvugu la kustahimili) na ambao walichaguliwa kuhamashisha jamii kuhusu mbinu ya Rais Museveni ya demokrasia shirikishi. Tuliwapa mafunzo na viinua mgongo kama vile fulana ya mikono (au T-shirts) na baiskeli, nao waliendeleza bidii ya uhamashishaji kwa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii na Wasaidizi wao yaani kwa kiingereza CDOs and CDAs (Community Development Officers and their Assistants).

Ukosefu wa wahamashishaji wakutosha waliopokea mafunzo ya kusisimua jamii ili ijisaidie yenyewe ni moja ya sababu zilizopelekea kuundwa na kupanuliwa kwa tuvuti hii na uundaji wa sehemu za mafunzo ziliomo. Nyingi ya mafunzo hayo ni miongozo ya kuandika vifaa vya mafunzo katika lugha mbali mbali huku ikizingatiwa mahitaji maalum katika jamii hiyo. Vifaa vya msingi vya mafunzo ni Mafunzo ya Kuimarisha, mtaala au mpangilio wa mafunzo ya uongozi wa jamii, na vijitabu vitatu vya wahamashishaji, juu ya (1) uhamashishaji, (2) kuleta mapato na (3) kufuatilia. kwa kuwa rasilimali kuu ambayo hutumika katika miradi ya kuwezesha jamii ni mafunzo ya uhamashishaji na uongozi, na wala sio kufadhili miradi ya jamii, vifaa hivi vya mafunzo ni nguzo muhimu katika shughuli hii.

Mafunzo ya Uongozi:

Moja ya vipengele vya maongozi ya miradi ya jamii ambayo inaitofautisha na mbinu za kawaida za uhamashishaji wa jamii, ni kuongezwa kwa mafunzo ya uongozi na usimamizi. Haitoshi tu kuruhusu au kusisimua jamii yenye mapato ya chini au iliyobaguliwa kushiriki katika maamuzi ya demokrasia na maendeleo; ni muhimu pia kwa jamii hiyo kuwa na uwezo wa kushiriki. Mafunzo ya uongozi na usimamizi imeundwa kwa kusudi la kuongeza uwezo huo.

Kama njia ya kukuza uwezo, mafunzo ya uongozi ni zaidi ya mafunzo ya kawaida, kwa kuwa yanatilia mkazo usambazaji wa ujuzi. Mafunzo ya uongozi yaliundwa miaka ya hamsini ya karne iliyopita na ilikusudiwa kutumiwa na wakurugenzi wakuu wa makampuni makubwa. Mafunzo hayo yalijumulisha usambazaji wa ujuzi, lakini pia yalisisitiza uhamashishaji, usambazaji wa habari, usaidizi na mageuzi (kupanga jinsi ya kufikia maamuzi na kutekeleza maamuzi hayo vizuri). Washiriki wetu walipenda kusema, "Hii sio tu mafunzo mbali kuwezesha, kuhamashisha na kupanga mikakati, mafunzo haya ni ya kuwezesha, kuhamasisha na kuwezesha."

Makadirio kwa Ushirikiano:

Ijapokuwa mhamashishaji ni lazima kwanza afanye makadirio ya rasilimali ya jamii, uwezo wake, vikwazo na matakwa yake, mbinu ya kipindi cha uhamashishaji inahitahitaji kuwa makadirio hayo lazima yahusishe jamii kwa jumla.. Sio lazima kuwa makadirio yote yatafanywa mara moja, mbali yawezwa kufanywa au kuendelea kufanywa na kikundi maalum cha jamii baada ya mradi huo kuanzishwa.

Mipango na miradi yote ya baadaye lazima itilie maanani mambo halisi yalivyo na wala sio mafikira au matakwa ya vikundi vya watu fulani katika jamii. Matakwa na uwezo wa jamii lazima utambuliwe na kila mtu katika jamii hiyo.

Kuamua Vipao Mbele; Matatizo na Malengo:

Wakati jamii imeunganishwa vya kutosha na kila kikundi kuhusishwa, wakiwemo wanawake, watu wenye elemavu na watu wengine ambayo ni vigumu kwao kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya jamii, basi itakuwa vyema kuzindua miradi ya jamii.

Hiyo hufanywa kwa kufikia makubaliano juu ya matatizo ambayo yatapewa kipao mbele na kutumia makubaliano hayo kutambua malengo ya muhimu ambayo yatapewa kipao mbele vile vile. Mbinu ya kuchangia mawazo ni moja ya vifaa vya kutumia hapa.

Mpango wa Utendaji Kazi wa Jamii (CAP):

Lazima jamii ikubaliane juu ya mambo ambayo ingependa kufanya katika muda fulani, kwa mfano katika kipindi cha mwaka mmoja, miaka mitano na kadhalika (kwa kawaida muda huo huwa sawa na kipindi cha mipango ya serikali katika wilaya hiyo). Mpango huo waweza kujumulisha moja au baadhi ya miradi ya jamii.

Jinsi ya kuandaa Kamati Kuu:

Kwa kuwa mambo yote ya miradi hayawezi kujadiliwa na kutimizwa katika mikutano ya baraza ya mamia ya watu, ni vizuri kwa jamii kuunda kamati kuu ya (Kamati ya Miradi, Kamati ya Maendeleo, CIC au Kamati Tekelezi ya Jamii). Kamati kuu lazima ichaguliwe kwa masikilizano ikiwa kupiga kura kutaleta migawanyiko; hapa mhamashishaji lazima awe anafahamu tamaduni na mazoea ya jamii hiyo.

Mhamashishaji atahitajika kuwafunza wanachama wa kamati kuu juu ya umuhimu wa kushirikisha jamii katika mipango, usimamizi na uongozi, ili kamati hiyo isigeuke na kuwa chama cha siri na kukosa uazi na uajibikaji kwa jamii kwa ujumla. Kamati kuu hiyo itarejelea na kurekebisha mpango wa utendaji kazi uliyoundwa, kuongezea mambo yanayohitajika, na kuunda mapendekezo ya miradi ili yaithinishwe na jamii (ni lazima mhamashishaji kusisitiza kwamba jamii ishirikishwe vilivyo). Hapa ni muhimu kutazama kwa makini mpango wa jamii wa usimamizi ( katika kipengele B) na kuiunganisha kwa hiki kipindi cha uhamashishaji.

Muundo wa Miradi ya Jamii:

Nguzo ya mafunzo ya uongozi ni kuuliza na kujibu maswali manne muhimu: (1) Je tunataka nini? (2) Je, tuna nini? (3) Tutatumiaje rasilimali tunayo ili kupata yale tunayotaka? na (4) Nini itafanyika ikiwa tutafanya hivyo? Haya hufafanuliwa kwa kina ili kuwa muundo wa mradi wa jamii. Hapa, kujibu kwa maswali hayo na kuunda mradi wa jamii, ni shirikishi, kwa kuwa inaongozwa na mhamashishaji kama mwalimu (ambaye anauliza maswali), na majibu kutolewa na washiriki kama kikundi (ambao wanajibu maswali).

"Mradi" ni kitendo (au msururu wa vitendo) ambacho kimeamuliwa na jamii (kama kikundi kilinacho hamasishwa na mhamashishaji). Mtindo wa muundu wa mradi in kitu kama hiki: Ni nini tatizo? Suluhisho la tatizo hilo ndilo litakalokuwa lengo; boresha lengo hilo ili liwe malengo madogo ambayo yanaweza kukadiriwa kwa urahisi (SMART); tambua rasilimali na vikwazo; buni mikakati ya kutumia rasilimali hiyo, epuka vikwazo hivyo, na afikia malengo yaliyowekwa; chagua mikakati ambayo italeta matokeo mema zaidi; amua jinsi mradi utakavyo endeshwa (viungo vyake, nani atafanya nini, bajeti, mpangilio); na uamue juu ya kufuatilia, kuripoti na kukadiria.

Majadiliano:

Mhamashishaji hapa atakuwa akitembea juu ya kamba konde. Kwa upande mmoja kuna wale watu wanaotegemea sana rasilimali kutoka nje; kwa upande mwingine kuna wale wana mahitaji ya kweli ya kuongezea rasilimali kutoka nje na ile ya jamii ili kutosheleza mahitaji yake (na ambayo huenda jamii ikawa na haki ya kupokea mchango fulani kutoka kwa serikali kuu au serikali ya wilaya). Ikiwa muundo wa mradi utatumiwa kama pendekezo la kuomba msaada, au ikiwa pendekezo litaandikwa na kamati kuu ya jamii, basi muundo wa mradi huo au pendekezo hilo litakuwa chombo cha majadiliano baina ya jamii na mashirika ya nje ambayo yanaweza kusaidia kwa rasilimali.

Hata ikiwa muundu wa mradi hautatatumika kutafutia rasilimali za nje, jamii hiyo inahitajika kuhakikisha kwamba mipango yake ni sambamba na mipango mingine katika sehemu na mazingira hayo, jamii zinazopakana nayo, wiliya au mkoa ambayo jamii hiyo ipo, mipango na vipao mbele vya kitaifa.. Mada hizi lazima zizingatiwe katika mijadala. Washika dau wote lazima wahushishwe kwenye mjadala huu. Muundo wa mradi ni chombo muhimu cha mashauriano wakati jamii inatafuta rasilimali na ufadhili au kibali cha serikali au yote mawili.

Utayarishaji wa Mkataba na Mashauriano:

Sio lazima kuwa na mkataba, lakini tunapendekeza hapa huwa ni vyema. Mhamashishaji anaweza kusaidia na kuongoza kamati kuu ya jamii kuandika mkataba kwa kuzingatia muundo wa mradi. Mkataba huo lazima uwe mfupi na wenye lugha rahisi, huku muundo wa mradi ukiambatanishwa.

Watakao tia sahihi mkataba huo lazima wawe wawakilishi wa washika dau wote, na hii yaweza kuafikiwa kwenye kipindi cha majadiliano ambayo imetajwa hapo juu.. Majadiliano huakikisha kwamba kuna uwazi kuhusu mradi uliopangwa, na kwamba wahusika wote (washika dau wote)wanaelewa malengo na mipango ya mradi wa jamii. Pia mijadala huonyesha kuwa jamii imejitwika jukumu la mradi huo.

Kutia Sahihi Mkataba:

Watakao tia saini mkataba ni pamoja na wawakilishi wa washika dau wote (kamati kuu ya jamii, wakuu wa wilaya, viongozi wa eneo hilo, maafisa wa mashirika, wahamashishaji). Mkutano ambapo mkataba utatiwa saini ni nafasi nzuri ya wahusika wote kukutana ana kwa ana kwa wakati mmoja. Hivyo basi ni nafasi njema ya mhamashishaji kuhakikisha kuwa jamii inahusika katika mradi wake (ushirika wa jamii) kama kipimo cha maendeleo.

Ikiwa kila mwenye kutia sahihi alikuwa amekubali kitambo kutia saini, basi utiaji wa sahihi unaweza kufanywa kama sherehe ambayo watu wote wanaweza kuhudhuria. Ijapokuwa wenye kutia sahihi wanaweza kupendelea kutia sahihi katika chumba cha ndani kama vile katika darasa, ni vyema zaidi ikiwa sahihi hizo zitatiwa mahali wazi kwa kuwa itaongezea uhalali wa mradi huo na kuboresha ufahamu kuhusu kuwezesha jamii.

Malipo ya Kwanza:

Ikiwa muundu wa mradi na mkataba umelenga kukusanya pesa kwa mradi wa jamii (kumbuka onyo kuhusu athari za kutegemea), basi wakati malipo ya kwanza yanapotolewa ni nafasi nzuri ya kufanya sherehe ya umma (labda hata ikiunganishwa na sherehe ya kutiwa saini mkataba).. Huu ni wakati wa kuinua hadhi ya mradi huo na kuimarisha ushirika wa jamii katika utekelezi wake.

Burudani, kwa mfano ya nyimbo, densi, kupiga ngoma na michezo ya kuigiza, inayofanywa na vikundi vya kitamaduni vya jamii hiyo, watoto wa shule au vikundi vya kujitolea, ni muhimu katika kuifanya watu kujivunia na kufurahia jamii yao na utamaduni wao. Vyombo vya habari vinaweza kualikwa ili tukio hilo litangazwe katika redio, gazetini na hata katika televisheni ya taifa.. Hii itachangia katika kuleta uwazi katika shughuli za mradi huo na kukuza ufahamu wa jamii kuhusu jukumu lake katika mradi huo.

Kuanza Kwa Utekelezi:

Katika kiwango hiki, jamii na viongozi wake, kama wanasiasa na wanahabari, watataka kuona vitendo na matokeo (kwa mfano ujengaji wa choo, usambazaji wa maji safi, hospitali au shule), na kwa hivyo wanapaswa kukumbushwa na kutiwa moyo kwamba kufuatilia na kuripoti lazima viende sambamba na vitendo. Ni katika kiwango hiki ambapo hamu na msisimko wa jamii inaweza kudidimia au kupotea kabisa haswa ikiwa vitendo (sana sana kuhusu mambo ya pesa) si ya uwazi au ikiwa watu wote katika jamii hawaelezwi mambo vizuri.

Ijapokuwa lengo kuu la jamii ni katika matokeo ya mwisho, lengo na mbinu ya mhamashishaji ni kuimarisha nguvu na uwezo wa jamii na kwa hivyo lazima aweke mkazo katika kufuatilia na kuripoti (kwa mdomo na maandishi). Pia, ni katika kiwango hiki ambapo jamii inagundua kuwa inahitaji ujuzi maalum inayohusiana na utekelzaji wa mradi huo (mambo ya fedha na uhasibu, kuandika ripoti na ufundi) na ambapo pia Kipengele B cha mikakati lazima kijumuishwe kwa kipindi hiki cha uhamashishaji.

Kufuatilia na Kuripoti:

Kufuatilia na kuripoti ni kutizama vitendo na shughuli za miradi ili kufanya marekebisho na kuepuka kufanya mambo ambayo hayakukusudiwa. Haya husaidiwa na makadirio ya kina ambayo huchunguza mambo kama vile matokeo ya vitendo, jinsi mradi ulivyoendeshwa, ikiwa mradi huo ilistahili kufanywa au la na mambo mengine ambayo yalifaa kupangiwa.

Hii huwezesha washiriki kurudia kipindi chote tena kwasababu ina malengo sawa na mipango na makadirio ya hapo mwanzo mradi ulipobuniwa.

Malipo ya Kufuatia:

Ikiwa kutakuweko na fedha zozote kutoka nje ambazo zinapewa jamii kupitia kwa kamati kuu, basi fedha hizo zinapaswa kutolewa katika awamu tofauti kulingana na matokeo ya matumizi ya awali.

Ijapokuwa hii haikuhitajika kutumiwa (katika mradi wa Uganda wa CMP Uganda) ni mfumo mzuri kama wa bima ili ikiwa kazi itasimamishwa (au ripoti isitolewe) basi vile vile fedha hazitatumwa. Hii huakikisha kuwa fedha zinatumika vizuri.

Kazi Inaendelea Hadi Mwisho:

Wakati kazi ikiendelea, mhamashishaji anajukumu la kuhakikisha kuwa ufuatilizi wa mradi unafanywa (haswa na wana chama wa jamii na washika dau wengine).Uwazi ni jambo muhimu kudumisha hamu na imani ya wanachama kwa kamati kuu haswa kwa mambo yanayohusu kiwango na aina ya matumizi ya pesa.

Fedha zinazotoka kwa mashirika ya nje lazima itegemee uwazi na uajibikaji (wa maelezo na ya kifedha) na kudumisha ukweli, uaminifu na uadilifu na wale waliopewa jukumu la kusimamia mradi.

Sherehe Rasmi ya Mwisho:

Ingawa sherehe na maadhimisho ni kama likizo kwa watu wengine, ni kazi ngumu sana kwa mhamashishaji. Kama vile sherehe ya kutoa fedha ambayo imeelezewa hapo mbele, sherehe ya mwisho ni nafasi ya kutangaza ufanisi wa mradi, kuhamashisha watu kuhusu uimarishaji wa jamii na kuhusu mradi huo uliokamilika, na kuthibitisha uhalali na manufaa ya kushiriki kwa jamii na kuwezesha jamii ya mapato ya chini.

Huku sherehe ya mwisho ikirembeshwa na wana habari na burudani, ni wakati mwema pia wa kukumbusha watu wa jamii hiyo kuwa wanahitajika kukadiria mradi uliokwisha na kuamua nini malengo yao mengine na hivyo basi kuanzisha tena kipindi kingine cha uhamashishaji.

Kurudia Kipindi Kizima:

Hii sio jambo la mara moja tu. Ni njia ya kuleta mabadiliko ya jamii (katika maendeleo) na lazima iendelezwe.. Ijapokuwa jamii itakuwa na uwezo wa kiwango cha juu kidogo kuliko vile ilivyokuwa kabla ya kipindi cha kwanza cha uhamashishaji, uhamashishaji wapaswa kuanzishwa tena. Pia, mhamashishaji atahitajika kuwafundisha watu wengine kuchukua nafasi ya wale watakao ondoka, na wahamashishaji pia lazima wateue na kufundisha wahamashishaji kutoka ndani ya jamii watakao kuwa na jukumu la kusisimua jamii na kuendeleza miradi wakati kikundi cha wahamashishaji wa kutoka nje kitakapo ondoka (na ambao hawatatumia ujuzu wa kuhamasisha kujinufaisha na kujitajirisha wenyewe kwa jasho la jamii bila kuimarisha uwezo jamii yenyewe).

Kila hatua ya kipindi cha uhamashishaji inahusiana na ile hatua iliyoitangulia na ile ifuatayo, na kwa kipindi chote kwa jumla. Kuna mpangilio na utaratibu fulani wa jinsi hatua hizo zinapaswa kutekelezwa. Kila wakati kipindi kinaporudiwa, kinarudiwa kwa kuzingatia makadirio na mapendekezo yanayotokana na kipindi cha awali na inajengwa juu ya mafanikio na uwezo uliopatikana kutoka kwa vipindi vya awali.

Miradi Mingine ya Kukuza Uwezo wa Jamii:

Miradi ifuatayo ni miongoni mwa mikakati ya uhamashishaji lakini inaweza kushirikishwa katika hatua tofauti kwenye kipindi cha uhamashishaji. Hii inawezwa kufanywa na mhamashishaji ikiwa tu anafahamu vyema mabadiliko ya mahitaji katika jamii.

Malengo ya uhamashishaji wa kujenga jamii yaweza kubadilika kutoka nchi moja hadi nyingine.. Hata hivyo, vipengele vinavyo fanana ni: kuondoa umaskini, uongozi bora, mabadiliko katika jamii (maendeleo), kuimarisha uwezo wa jamii, kuimarisha uwezo wa watu wa mapato ya chini na wale waliobagulia au kutengwa, na usawa wa kijinsia.

  • Kabla, wakati mradi ukiendelea na baada ya kila kipindi cha mradi, ni muhimu kufanya utafiti na kukadiria aina na malengo ya mashirika yote yalioko kwenye jamii hiyo (kama vile baraza la wazee na mabaraza mengine, vikundi vya wamama, vikundi vya kupeana mkopo, vugu vugu la watu, mashirika ya vikundi maalum kwa mfano;mashirika ya watu wenye ulemavu au wanyonge);
  • Kujenga na kuimarisha mashirika ya eneo la jamii iliyolengwa (kwa mfano kwa kuhakikisha kwamba kuna uwakilishi na ushirikiano wa jamii), kuimarisha kushiriki kwa jinsia zote hasa wanawake, na kusaidia katika kusajiliwa kwa makundi hayo;
  • Kukuza ushirikiano wa kikazi kati ya mashirika tofauti: kuendeleza nafasi za kukusanya, kutumia na kuwianisha rasilimali (ya kibinadamu, fedha, vifaa na shamba/ardhi);
  • Kuimarisha mbinu za kuzalisha mapato na kazi, kwa kusisiza mafunzo, kupeana mikopo na mauzo;
  • Kuboresha makazi na muundo msingi;
  • Miradi ya mazingira (kwa mfano kukuza uwezo wa jamii kudhibiti uchafu na takataka na kutunza mali ya asili); na
  • Kushiriki kwa jamii katika kudhibiti na kupunguza janga (kambi za wakimbizi, kupata makazi mapya na kutegeneza upya).
––»«––

Kwa Maonyesho ya Power Point ya kipindi cha uhamashishaji, ikiwa ni maandishi pamoja na michoro yake, tazama Maonyesho ya Power Point.


© Hakimiliki 1967, 1987, 2007 Phil Bartle
Web Design: Lourdes Sada
––»«––
Imeratibishwa mwisho: 11.11.2011

 Nyumbani

 Uhamashishaji